Friday, December 27, 2013

NAOMBA NIKUJUZE YA KWAMBA TABU LEY, MKALI WA RHUMBA AMEACHA WATOTO 68


Kama kuna mwanamuziki ambaye ameacha historia ya pekee katika maisha yake, si mwingine ni Pascal-Emmanuel Sinamoyi au Tabu Ley (76) kama anavyojulikana na wengi.
Alifahamika pia kwa majina ya Mfalme wa Rhumba Afrika au muimbaji mweye sauti nyororo, ambaye amefariki dunia na kuacha watoto 68 na wajane wasiojulikana idadi.
Ana historia yenye matukio lukuki katika uhai wake, miongoni mwa matukio hayo ni kuzaliwa na kupewa jina la Pascal-Emmanuel Sinamoyi Tabu, lakini baada ya Joseph-Desiré Mobutu kuchukua uongozi wa nchi na kubadili jina la nchi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kuiita Zaire, pia na yeye (Mobutu) kubadili jina lake na kujiita Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Za Banga, Wazaire wengi walibadili majina akiwemo yeye (Tabu), aliyejiita Tabu Ley.
Matukio ya Tabu Ley hayakuishia hapo pia alizaliwa Novemba na amefariki dunia Novemba (Novemba 13 1937- Novemba 30 2013), historia ya maisha yake ya ndoa inaonyesha alimuoa Mbilia Bel na kuzaa naye mtoto mmoja, lakini baada ya kifo chake Tabu Ley anatajwa kuacha watoto 68 akiwemo rapa wa Ufaransa Youssoupha.
Tabu Ley mwaka 1988 alikwaruzana na Mobutu sese Seko na kulazimika kuikimbia Zaire na kwenda kuishi uhamishoni Ufaransa. Mwaka 1985 Serikali ya Kenya ilipiga marufuku muziki wa kigeni kwenye redio ya Taifa, lakini Tabu Ley akimshirikisha Mbilia Bel waliimba wimbo “Twende Nairobi” uliokuwa ukimsifu Rais Daniel arap Moi, baada ya muda mfupi Rais Moi aliruhusu tena nyimbo za kigeni kwenye redio ya Taifa.
Kati ya watu wanaotajwa kuwa kiini cha kumbukumbu wakati huo, ni pamoja Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu wa Za Banga, Rais wa zamani wa iliyokuwa Zaire na mwanamuziki wa Rhumba, Pascal-Emmanuel Sinamoyi Tabu Ley pia wa Zaire.
Mobutu anakumbukwa kwa utawala wa kidikteta na kuiongoza Zaire, sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kama familia yake na siyo nchi. Mwanamuziki Pascal maarufu kama Tabu ley akikumbukwa kwa mafanikio katika sanaa ya muziki Afrika.
Tabuley, aliyezaliwa mjini Bagata Novemba 13 1937, na ambaye anabaki kuwa alama na kielekezo cha mafanikio na kiini cha utambuzi wa muziki wa Afrika katika mtindo wa ‘Soukous’, amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Historia ya muziki inamuonyesha Tabuley ni mwanzilishi na mmiliki wa kundi la Orchestre Afrisa International, alifariki dunia Novemba 30 mwaka huu jijini Brussels, nchini Ubelgiji alikolazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa kiharusi.
Tabu Ley, aliyekuwa pia mwanasiasa hakuwahi kupata nafuu tangu alipokumbwa na ugonjwa wa Kiharusi mwaka 2008, na afya yake ilibadilika zaidi Jumatatu ya wiki iliyopita kabla ya kufariki dunia.
Msanii huyo alikuwa akitarajiwa kufanyiwa mazishi ya kitaifa kwenye Jiji la Kinshasa Jumatatu wiki ijayo, alisema mmoja ya wakwe zake, Jean-Claude Muissa.
Hakuna shaka kwamba msiba wa mkongwe huyo umewashtua makundi ya watu wote, wakubwa kwa wadogo hasa ukizingatia kuwa, muziki wake umeendelea kupendwa hata kizazi baada ya kizazi.
Jitihada zake za kuutangaza muziki wa Kongo na kuufanya kujulikana kimataifa, zitabaki kuwa changamoto na mfano wa kuigwa hasa kwa kuzingatia ‘utajiri’ mkubwa wa nyimbo alizoacha 3,000 na albamu zaidi ya 250.
Tabu Ley anabaki kwenye kumbukumbu ya mwanamuziki pekee wa Rhumba Afrika aliyeimba kwa mafanikio, akitumbuza jukwaa kwa zaidi ya miaka 50, huku sehemu kubwa ya nyimbo zake akiwa ametunga mwenyewe.
Mbali na kuwa na uwezo wa kuimba nyimbo kwa lugha zaidi ya moja, pia alitunga na kuimba nyimbo za Kiingereza na hiyo ilithibitika mwaka 1990, alipohamia California, Marekani na kuendesha shughuli zake za muziki.
Baadaye Tabu Ley alikuja kuwa mpinzani mkubwa wa utawala wa Mobutu Sese Seko uliodumu kuanzia mwaka 1965 mpaka 1997 kiasi cha kulazimika kuikimbia nchi na kwenda kuishi uhamishoni.
Mwaka 1990, Mobutu aliupiga marufuku wimbo wa Tabu ley “Trop, c’est trop” ikimaanisha kwa tafsiri isiyo sahihi ‘Imezidi, imetosha’.
Baada ya Rais Mobutu Sese Seko kuondolewa madarakani mwaka 1997, Tabu Ley alirejea Kinshasa na kupewa nafasi kwenye Baraza la Mawaziri kwenye Serikali ya Rais Laurent Kabila.
Aliteuliwa kuwa Waziri wa Utamaduni wakati wa utawala wa hayati Rais Laurent-Desire Kabila---baba wa Rais wa sasa Joseph Kabila, na baadaye akawa Makamu Gavana wa Kinshasa.
MUZIKI:
Mwaka, 1954, wakati akiwa na miaka 14 aliandika wimbo wake wa kwanza iliyojulikana kama ‘Bessama Muchacha’ akishirikiana na Joseph “Le Grand KallĂ©” wa bendi ya Kabasele na African Jazz.
Baada ya kumaliza sekondari, alikuwa tayari mwanamuziki kamili jukwaani. Tabu Ley aliimba nyimbo nyingi za ukombozi wakati huo, na kibao chake kilichotamba kilijulikana kama Cha Cha baada ya Zaire kupata uhuru 1960.
Alibaki kwenye bendi ya African Jazz mpaka mwaka 1963 baada ya kukubaliana na Nico Kasanda kuunda kundi lao lililojulikana kama African Fiesta.
Kundi hilo lilidumu kwa miaka miwili tu baada ya wawili hao kutengana, ambapo Tabu Ley aliunda kundi lingine kutoka kwenye muungano huo na kulipa jina la African Fiesta National, ambalo pia lilikuwa linajulikana kama African Fiesta Flash.
Baadhi ya nyimbo walizopiga ni pamoja na Afrika Mokili Mobimba uliouza nakala za kutosha miaka ya 1970.
Wanamuziki wengine kama Papa Wemba na Sam Mangwana ni miongoni mwa waliokuwa kwenye kundi hilo miaka ya 1970.
Mwaka 1970, Tabu Ley alianzisha kundi la Orchestre Afrisa International, ambapo aliwahi kuimba pamoja na Franco Luambo wa TPOK Jazz na kufyatua vibao kama “Sorozo”, “Kaful Mayay”, “Aon Aon”, na “Mose Konzo” na Iisanga ya Baganga.
Kutokana na nyimbo zake kama “Adios Thethe” na “Mokolo nakokufa” (siku yangu ya kifo), Tabu Ley alichangia kuusambaza umaarufu wa mtindo Soukous mwaka 1970, na alikuwa Mwafrika wa kwanza kutumbuiza kwenye ukumbi mashuhuri wa Olympia, Paris Ufaransa.
UHUSIANO NA MBILIA BEL
Baadaye Tabu Ley aligundua kipaji cha msanii wa kike Mbilia Bel, ambaye kufanya kwake kazi kwenye kundi hilo kulisaidia kwa kiasi kikubwa kuitangaza bendi yake. Alimfanya Mbilia Bel kuwa mwanamke wa kwanza kuimba midundo ya soukous iliyozidi kupendwa zaidi.
Uhusiano wa karibu kati ya Mbilia Bel na Tabu Ley ulisababisha kufunga ndoa katikati ya miaka 1980. Mwaka 1987, Tabu Ley alimleta msanii mwingine wa kike Kishila Ngoyi (Faya Tess) kusaidia kuimba na Mbilia Bel.
Kujiunga kwa Tess kwenye kundi hilo kulipelekea uhusiano wa Mbilia Bel na Tabu Ley kuyumba, huku msanii huyo mpya akimfunika vilivyo Mbilia Bel katika ziara ya muziki walizofanya Tanzania, Kenya na Rwanda kuitangaza albamu ya Nadina.
Mwishoni mwa 1987, Mbilia Bel alijiondoa kwenye kundi na kuamua kufanya muziki kama msanii huru, hatua iliyoporomosha umaarufu wa kundi la Tabu Ley.

No comments:

Post a Comment

Blogger Widgets