Wednesday, January 9, 2013

Ngono inasababisha saratani ya kizazi


UTAFITI mpya wa kitabibu umebaini kuwa saratani ya shingo ya kizazi, inasababishwa pamoja na mambo mengine na ngono kama ilivyo kwa ugonjwa wa Ukimwi, madaktari bingwa wa magonjwa ya maradhi hayo wamesema.
Hayo yalielezwa na daktari bingwa wa uchunguzi wa magonjwa katika Kitengo cha Patholojia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Henry Mwakyoma na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk Crispin Kahesa.
Madaktari hao wametaja mambo mengine yanayoweza kusababisha saratani ya shingo ya kizazi kuwa ni kujiingiza kwenye mapenzi katika umri mdogo, kuolewa mara nyingi, kuwa na wapenzi wengi, kusafisha sehemu za siri kwa bidhaa zenye kemikali na kuzaa mara nyingi.
Katika kiwango cha kimataifa, wastani wa mwanamke kuzaa bila kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa wa saratani, ni watoto wanne.
Dk Mwakyoma alisema saratani ya shingo ya kizazi inatokana na aina 40 ya virusi, aina mbili ikiwa ni virusi vinavyosambaa kwa njia ya ngono... “Human papilloma virus (HPV) Squamos cell carcinoma kirusi namba 16 na Adenocarcinoma namba 18, ni kati ya virusi 40 vinavyosababisha saratani ya kizazi na vyenyewe vinachangia tatizo hilo kwa asilimia 70.”
Alisema saratani ya uzazi ndiyo inayoongoza ikilinganishwa na nyingine nchini na asilimia 80 ya wagonjwa, wameambukizwa kwa ngono.
“Saratani hiyo husambaa kwa ngono kutoka mwanamke mmoja kwenda kwa mwingine. Mwanamke mwenye saratani ya kizazi akifanya ngono, mwanamume huchukua virusi na kumwambukiza mwingine atakayefanya naye ngono,” alisema na kuongeza:
“Wagonjwa wengi na wale ambao tayari wana maambukizi, wamekuwa wakikutwa na virusi hawa wa aina mbili ambao wamekuwa wakienezwa zaidi kwa njia ya zinaa. Inawezekana mwanamume akawa ametoa kirusi kwa mwanamke mmoja kwenda kwa mwingine.”
“Hata hivyo, kuna wanaume ambao tayari wameshakuwa na maambukizi ya HPV wanatembea na virusi, hawa tunawaita (high risk sexual male patner) wanaume hawa utakuta kila akioa mke anakufa kwa saratani ya shingo ya uzazi, lakini kamwe virusi hao hawawezi kumwathiri yeye.”
Alisema kuanza ngono mapema nako kunachangia kwa kiasi kikubwa maambukizi ya saratani hiyo, kwani binti anakuwa katika hatari zaidi ya kupata maambukizi mapema na hivyo kuweza kumwathiri mapema zaidi, tofauti na yule aliyeanza baadaye.
“Idadi kubwa ya wanawake wamekutwa na saratani mapema sana, ukilinganisha na umri wao, lakini wengi wao wamekuwa wakikutwa na ugonjwa huu kuanzia umri wa miaka 35 kwenda juu. Hii inamaanisha kuwa walipata maambukizi hayo walipokuwa na miaka 20-25.”
Dk Mwakyoma alisema licha ya hivyo mgonjwa anaweza asitambue tatizo hilo mpaka miaka 10 hadi 15 baadaye ambapo tatizo linajitokeza hadharani.

Chanzo: Mwananchi.

No comments:

Post a Comment

Blogger Widgets