
Kipa Ospina asajiliwa Arsenal
*Mourinho aubeza mshahara wa Shaw
* Ferdinand aanza Queen Park Rangers
Wakati Arsenal wamekamilisha usajili wa golikipa wa Timu ya Taifa ya
Colombia, David Ospina, Queen Park Rangers (QPR) wameanza kupata huduma
za mabeki wa kati Rio Ferdinand na Steven Caulker huku Jose Mourinho
akimvaa Luke Shaw.
Arsenal wamefanikisha usajili wa kipa ambaye aliruhusu mabao machache
zaidi katika hatua za makundi kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini
Brazil majuzi, taarifa hiyo ikiwa imetolewa na kocha wa klabu yake ya
Nice, Claude Puel.
Ospina (25) amekuwa na klabu hiyo ya Ufaransa tangu 2008 na alisaidia
nchi yake kufika hatua ya robo fainali na kocha Puel alisema Arsenal
watafurahi kwani Ospina ni kipa mzuri sana.
Pasipo kuthibitisha usajili huo, Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger
alijibu swali la waandishi wa habari kwa kusema aliamini kwamba kipa
huyo alifanya vyema sana kwenye michuano ya Kombe la Dunia.
Wenger amepata kunukuliwa akisema kwamba kuna uwezekano wa Ospina
kumpoka namba kabisa kipa namba moja wa Arsenal, Mpolishi Wojciech
Szczesny. Ospina alicheza dakika zote za mechi zote za Colombia na nchi
hiyo iliruhusu pia mabao machache zaidi miongoni mwa timu za Amerika
Kusini wakati wa mechi za kufuzu.
Ospina ndiye alichukua mikoba ya Hugo Lloris aliposajiliwa na Tottenham Hotspur kutoka Lyon lakini kabla ya hapo alikuwa Nice.
MOURINHO ASEMA SHAW GHALI MNO
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho ameendelea kuzungumzia masuala ya
wachezaji wa timu nyingine, akiwashangaa Manchester United kumsajili
beki wa kushoto wa Southampton ambaye ni ghali sana.
Mourinho amedai kwamba madai ya mshahara mkubwa ya Shaw yangeweza
‘kuiua’ Chelsea. Shaw alisajiliwa kwa pauni milioni 27 na amekuwa
akiwaniwa na timu nyingi, ikiwa ni pamoja na Arsenal na Liverpool.
Mreno huyo amedai Shaw kulipwa pauni 100,000 kwa wiki ni kiasi
kikubwa mno, lakini Kocha wa Manchester United, Louis van Gaal amedai
kwamba atakaa faragha na Mourinho kuzungumzia suala hilo.
“Tukimlipa kijana mwenye umri wa miaka 19 kile tulichotakiwa kumlipa,
basi kumsajili Luke Shaw kungetuua. Tungeua uthabiti wetu huku
tukitakiwa kuzingatia uungwana katika matumizi ya fedha, sasa ukimlipa
kijana mdogo kiasi hicho basi kesho yake wengine watakuvamia kutaka
nyongeza,” akasema Mourinho.
Mourinho anajenga hoja kwamba si sahihi mchezaji mpya na mwenye umri
mdogo kiasi hicho kulipwa kuliko wakongwe ambao wamechezea klabu mechi
hadi 200, kuiletea mataji na sifa nyingi.
FERDINAND, CAULKER WAANZA KAZI QPR
Mabeki wapya wa kati wa Queen Park Rangers (QPR), Rio Ferdinand na
Steven Caulker wameanza rasmi majukumu katika klabu hiyo iliyopanda
daraja msimu huu baada ya kuwa imeshuka msimu uliopita.
Waingereza hao wawili walicheza dakika 45 kila mmoja katika mechi ya
kirafiki nchini Ujerumani kwa ajili ya kujiandaa na Ligi Kuu ya England
inayoanza mwezi ujao. Ferdinand alianza kufundishwa soka ya kulipwa na
kocha wa sasa wa QPR, Harry Redknapp.
Katika hatua nyingine, QPR wameamua kumrejesha kipa wao, Julio Cesar
(34) wa Brazil aliyekuwa ametolewa kwa mkopo katika klabu inayocheza
Ligi ya Marekani ya Toronto FC. Kipa mwingine katika QPR ni Mwingereza,
Robert Green.
Wakati huo huo, West Ham United wamepata pigo kubwa, baada ya
mshambuliaji wao wa kutegemewa kuumia enka na hivyo atakuwa nje ya dimba
kwa miezi karibu minne, ikimaanisha ataanza kucheza Novemba.