Monday, January 27, 2014

JAMAA ABANIKWA KWENYE MOTO SIKU 2 KAMA KITOWEO BAADA YA KUTUHUMIWA KUIBA PIKIPIKI


Mkazi wa Mjimwema wilayani Mufindi mkoani Iringa, Ezekiel Kaganga (29), amekamatwa na watu wanaomtuhumu kwa kuiba pikipiki ya biashara maarufu bodaboda, na kumbanika kwenye moto kama kitoweo.

Akisimulia unyama huo jana, Kaganga ambaye amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mufindi mjini Mafinga, alisema anafahamiana na watuhumiwa hao na kabla ya tukio hilo, Januari 7, mwaka huu walikuwa pamoja wakinywa bia katika moja ya maduka ya kuuzia pombe mjini Mafinga.

Alisema  kesho yake, Januari 8, mwaka huu alipokea taarifa kuwa katika duka hilo la pombe lililopo katika eneo la Mashine ya Mpunga, kuna pikipiki ilipotea katika mazingira ya kutatanisha baada ya yeye kuondoka.

Kwa mujibu wa Kaganga, mmoja wa watu waliokuwa wakimtuhumu kuhusika na wizi huo, alimfuata na kumtaka arejeshe pikipiki hiyo, na yeye akamjibu kuwa hajui lolote kuhusu kupotea kwa pikipiki hiyo.

“Jamaa hawakuridhishwa na majibu yangu na Ijumaa ya Januari 12 nilikamatwa na polisi nikihusishwa na wizi huo na baada ya kukosekana ushahidi, nilitolewa Januari 17,” alisema Kaganga.

Siku tatu baada ya kutoka Polisi, Kaganga alikamatwa na vijana hao na kupelekwa katika msitu wa Lumwago nje kidogo ya Mji wa Mafinga.

Katika msitu huo alifungwa kamba, kupigwa viboko na baadaye alining’inizwa juu ya mti huku moto ukiwa umewashwa chini yake.

“Nilibanikwa kama kuku, moto ukiwa chini mie nikiwa nimefungwa juu ya mti; niliachwa hapo kwa siku mbili,” alisema.

Alisema baada ya siku mbili alihamishwa kutoka katika msitu huo na kupelekwa eneo la Machinjio mapya na kumwagiwa mafuta ya taa ili achomwe na moto na kundi la watu wanaokadiriwa kuwa saba.

Alidai akiwa mahututi kabla ya kuchomwa moto, kulitokea mabishano kati ya watuhumiwa wengine wakishauri aachwe bila kuchomwa moto, wakaamua kumuacha ambapo baadaye kidogo alichukuliwa na wasamaria wakampeleka kituo cha Polisi.

Sehemu ambazo amejeruhiwa zaidi ni mgongoni, makalioni, mikononi, ubavuni, miguuni na shingoni.

Kaka yake Kaganga, Isaac alisema mdogo wake anaendelea kupata matibabu, na hali yake sio mbaya sana japokuwa hawezi kutembea.

Alisema alipata taarifa ya kupotea kwa mdogo wake kulikokuwa kukihusishwa na wizi wa pikipiki, akawaomba  watuhumiwa wasimdhuru mdogo wake, badala yake wamsubiri  arudi kutoka safarini Arusha ili alipe pikipiki hiyo.

“Hata hivyo vijana hao hawakuwa na subira na badala yake wakamfanyia unyama waliofanya,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi amesema tayari watu wawili wanashikiliwa Polisi  wakihusishwa na tukio hilo la kinyama.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Alex Ludago (28) na Steven Michael (29) wote wakazi wa MET mjini Mafinga.
Credit- ziro99blog  

No comments:

Post a Comment

Blogger Widgets