MWANAMKE aliyetajwa kwa jina moja la Winfrida ambaye ni mke wa mtu amekwaa aibu ya karne baada ya kudaiwa kutaka kuuza kiwanja ambacho si mali yake na kujipatia fedha isivyo kihalali kutoka kwa mtu aitwaye Stanlaus Hajj ‘Stan’, Ijumaa lina mkanda kamili.
Awali ilidaiwa kuwa mwanamke huyo, alichukua Sh. milioni tano kama malipo ya awali alinasa katika mtego wa polisi wa Kituo cha Kijitonyama ‘Mabatini’, Dar alipokuwa akifuatilia Sh. milioni 15 ili aweze kuuza kiwanja hicho kwa Sh. milioni 20.
Madai hayo yapo katika Kituo cha Polisi cha Kijitonyama ‘Mabatini’ jijini Dar baada ya mwanamke huyo kuwekewa mtego na kunasa maeneo ya Mlimani City.
Ilielezwa na mashuhuda wetu kwamba mwanamke huyo ambaye ni mkazi wa Bagamoyo, Pwani alinaswa baada ya kuwekewa mtego na polisi alipotaka kuchukua fedha hizo.
Akizungumza na waandishi wetu, Stan alisema mwanamke huyo alimwonesha kiwanja maeneo ya Bunju, Dar ambacho alitaka amuuzie kwa Sh. milioni 20.
“Tulienda Bunju akanionesha kiwanja tukakubaliana bei lakini akaniambia nimpatie milioni tano kwanza kwa kuwa alikuwa na shida na ada za watoto wake, tukaandikishiana nikampa,” alidai Stan.
Alidai kuwa, baada ya siku mbili alikwenda kukiangalia kiwanja hicho akiwa na rafiki yake aitwaye Kassim Rashid lakini wakashangaa kumkuta mlinzi, walipojieleza wakaambiwa kuwa wametapeliwa.
Alisema kuwa mlinzi huyo aliwaambia kuwa eneo hilo siyo la mwanamke huyo kwani ameshawauzia watu wengi kiwanja hicho na kuwataka waondoke.
“Nilichanganyikiwa lakini rafiki yangu akanipa moyo na ushauri kuwa nikatoe taarifa katika Kituo cha Polisi cha Wazo ambako nilifungua jalada la kesi namba WH/RB/494/2014 -KUJIPATIA PESA KWA UDANGANYIFU,” alisema Stan.
“Kassim alinishauri nimpigie simu mama yule na kumwambia fedha iliyobakia nitampa baada ya siku tatu ili kumvuta tumkamate kama tulivyofanya leo (Jumanne wiki hii),” alisema.
Baada ya siku tatu, mtego wa kumnasa mwanamke huyo ukapangwa baada ya kumtaka afike kuchukua fedha zake zilizobaki.
Stan na mwanamke huyo walipanga kukutana katika Baa ya Msumbiji ilioyopo maeneo ya Mlimani City ambako Stan alikuwa amejipanga akiwa na polisi wa Kituo cha Kijitonyama (Mabatini).
“Nawashukuru polisi hasa Mkuu wa Upelelezi, Ezekiel pamoja na Mkuu wa Kituo, Mapunda maana baada ya kuwapa ile RB ya Wazo walinipa ushirikiano mkubwa sana na wakanipa gari na kufanikisha kumtia mbaroni yule mwanamke,” alisema Stan.
Mwanamke huyo alipofika eneo walilopanga kukutana na Stan alinaswa katika mtego huo kisha kusweka rumande Mabatini kusubiri sheria ichukue mkondo wake.
No comments:
Post a Comment